Wananchi wa Morocco waendeleza maandamano
Polisi Morocco wamepambna na waandamanaji wanaoipinga serikali katika eneo la Rif, ambalo limekumbwa na maandamano ya siku kadhaa ya wananchi wanapinga kukamatwa mwanaharakati maarufu.
Maandamano hayo yaliibuka Ijumaa baada ya vijana waliokuwa na hasira kuwarushia mawe na takataka polisi katika mji wa Imrouren, yapata kilomita 450 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Morocco, Rabat.
Polisi wametumia maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakilalamikia ufisadi, ukandamizaji na ukosefu wa ajira.
Maandmano hayo yamekuja baada ya polisi kumkamata Nasser Zefzafi, ambaye anaongoza maandamano ya kupinga ufisadi. Anashikiliwa kwa tuhuma za kuwa tishio kwa usalama wa taifa kati ya mengine.
Katika mji wa al Hoceima alikokamatwa Zefzafi, maduka mengi yalifungwa Ijumaa kufuatia mgomo ulioitishwa na wapinzani wa serikali.
Maandamano ya kupinga ufisadi yamekuwa yakifanyika nchini Morocco tokea mwaka jana wakati mchuuzi wa samaki alipokanyagwa na lori la kubeba taka wakati akijaribu kuchukua samaki wake waliokuwa wamechukuliwa na maafisa wa polisi kwa sababu alikuwa akiuza bidhaa sehemu isiyotakiwa.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema polisi imewakamata waandamanaji 71 katika siku chache zilizopita.
Wanaharakati wanasema maandamano ya sasa ni muendelezo wa mwamko wa watu wa Morocco ulioanza sambamaba na mwamako wa watu wa Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati mwaka 2001 na kupelekea madikteta kadhaa kuangushwa.
Kuna umasikini mkubwa na ukosefu wa ajira Morocco, nchi ambayo imekuwa ikitawaliwa na mfumo wa ufalme kwa miaka 350 sasa.