Rais wa Kongo DR: Sikuwahi kuahidi uchaguzi, lakini ninaupa umuhimu mkubwa
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa, hakuwahi kuahidi chochote kuhusiana na kuandaa mchakato wa kufanyika uchaguzi wa rais mwaka huu nchini.
Rais Kabila ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la Der Spiegel la Ujerumani na kuongeza: "Sikuwahi kuahidi lolote kabla, lakini ninatumai kwamba taratibu zitachukuliwa kwa lengo la kufanyika uchaguzi huo haraka iwezekanavyo." Aidha rais Kabila ameongeza kuwa: "Tunataka uchaguzi sahihi, sio ilimradi uchaguzi" na sasa serikali iko katika taratibu za kusajili wapiga kura na zoezi hilo linaendelea vizuri. Itakumbukwa kuwa, katika makubaliano yaliyofanyika kwa lengo la kuhitimisha mvutano nchini humo na kusimamiwa na Kanisa Katoliki, Rais Kabila aliahidi kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka huu 2017.
Mwezi Aprili mwaka huu Rais Kabila alitangaza kuwa uchaguzi huo utafanyika katika tarehe iliyopangwa huku miezi miwili kabla Waziri wake wa Bajeti Pierre Kangudia akisema kuwa, ni vigumu kufanyika uchaguzi huo kutokana na gharama kubwa sawa na kiasi cha dola bilioni 1.8. Aidha Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amezungumzia mabadiliko tarajiwa ya katiba nchini humo ambayo yanatajwa kuwa yatampa mwanya na fursa rais huyo kuweza kugombea tena kwa muhula wa tatu katika uchaguzi ujao na kusema, binafsi hana nia ya kutia doa katiba ya taifa hilo.
Matamshi ya Rais Joseph Kabila ya kuheshimu katiba na kuitisha uchaguzi katika tarehe iliyopangwa, yamekuja ikiwa ni siku mbili zimepita tangu Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilipotoa mwito kwa viongozi wa nchi za Kiafrika kumshinikiza Rais Joseph Kabila aitishe uchaguzi wa rais nchini humo. Mgogoro wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliibuka baada ya kuahirishwa tarehe ya uchaguzi wa rais na kadhalika sisitizo la Rais Joseph Kabila la kutaka kuendelea kusalia madarakani nchini humo.
Licha ya kutiwa saini makubaliano baina ya wapinzani na serikali juu ya kufanyika uchaguzi wa rais tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu, hata hivyo inaonekana kuwa, uchaguzi huo hautaweza kufanyika katika tarehe iliyopangwa.