Mrengo wa waasi Sudan Kusini wasaini mapatano ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30056-mrengo_wa_waasi_sudan_kusini_wasaini_mapatano_ya_amani
Kundi la waasi la Sudan Kusini katika Jimbo la Yei River limesaini makubaliano ya amani na serikali ili kumaliza mapigano yaliyosababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2017 01:59 UTC
  • Mrengo wa waasi Sudan Kusini wasaini mapatano ya amani

Kundi la waasi la Sudan Kusini katika Jimbo la Yei River limesaini makubaliano ya amani na serikali ili kumaliza mapigano yaliyosababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Brigedia Jenerali Hillary Yakani kwa niaba ya kundi la waasi la Sudan People's Liberation Army In Opposition (SPLA IO) na Meja jenerali Marshal Babanen kwa niaba ya serikali. Tukio hilo limeshuhudiwa na waziri anayeshughulikia maswala ya baraza la mawaziri na majenerali kutoka pande zote mbili. Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo ya siku nne, kundi la SPLA IO limetangaza kuacha mapambano kuanzia leo.

Rais Kiir wa Sudan Kusini

Meja Jenerali Yakani amesema wataendelea kuwashawishi wenzao ambao bado wapo kwenye uasi kujiunga na mchakato huo ili kuijenga nchi. Kwa mujibu wa Meja Jenerali Marshal Babanen makubaliano hayo yanatarajiwa kuanza kutekelezwa ndani ya wiki 18.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimeshasababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.