Rwanda yaendeleza juhudi za kuwarejesha raia wake nchini tangu vita vya 94
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30074-rwanda_yaendeleza_juhudi_za_kuwarejesha_raia_wake_nchini_tangu_vita_vya_94
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, tayari limesharejesha maelfu ya wakimbizi wa Rwanda waliokimbia vita vya mwaka 1994, nchini mwao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2017 09:42 UTC
  • Rwanda yaendeleza juhudi za kuwarejesha raia wake nchini tangu vita vya 94

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, tayari limesharejesha maelfu ya wakimbizi wa Rwanda waliokimbia vita vya mwaka 1994, nchini mwao.

Erika Fitzpatrick, naibu mkuu wa idara ya habari ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) nchini Rwanda amesema kuwa, shirika hilo linaendelea na juhudi za kuwarejesha nyumbani wakimbizi elfu 20 wa nchi hiyo ndani ya mwaka huu 2017. Awali shirika hilo lilipitisha mpango wa kutoa msaada wa kifedha kwa wakimbizi wa Rwanda wanaokubali kurejea nchini kwao kwa hiari na kwamba mpango huo utaendelea hadi mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu.

Wakimbizi wa Rwanda wakati wa mauaji ya mwaka 1994

Hii ni katika hali ambayo serikali ya Kigali nayo imekuwa ikiwashawishi raia wake wanaoishi ugenini kurejea nchini. Wizara ya Kukabiliana na Majanga na Masuala ya Wakimbizi nchini Rwanda imetangaza kuwa, kati ya mwaka 1994 na 2014, zaidi ya wakimbizi milioni tatu na laki nne walikuwa wamerejea kwa hiari nchini kwao. Raia wa Rwanda walikimbia nchi hiyo mwaka 1994 baada ya kuibuka mauaji ya halaiki yaliyosukumwa na ukabila ambapo karibu watu milioni moja waliuawa.