Rais wa Somalia alionya kundi la al-Shabab; aahidi kulipiza kisasi
Rais wa Somalia amelionya kundi la wanamgambo wa kitakfiri na kigaidi al-Shabab na kusema kuwa, jeshi la nchi hiyo litatoa jibu mwafaka kwa hujuma za kigaidi za wanamgambo hao.
Rais Mohamed Abdullahi Mohamed ameashiria shambulio la jana la kigaidi la kundi la kitakfiri la al-Shabab kaskazini mashariki mwa nchi hiyo lililopelekea kuuawa na kujeruhiwa makumi ya wanajeshi wa nchi hiyo na kusema kuwa, hatua zilizo dhidi ya ubinadamu za wanamgambo wa al-Shabab hazitaachwa bila majibu bali vikosi vya nchi hiyo vitalipiza kisasi kwa wanamgambo hao.
Rais wa Somalia amesema kuwa, katika shambulio hilo la jana la magaidi wa al-Shabab idadi kadhaa ya wanajeshi wa nchi hiyo pia wametekwa nyara na wanamgambo hao.
Rais Mohamed Abdullahi Mohamed ambaye serikali yake inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya ukosefu wa usalama amesisitiza kwamba, serikali ya Mogadishu imeazimia kukabiliana kwa nguvu zake zote na wanamgambo wa al-Shabab.
Wakati huo huo, huku idadi ya waliouawa katika shambulio hilo la jana ikitajwa kuwa ni 38, kundi la wanamgambo wa al–Shabab limedai katika taarifa yake kwamba, limewauwa askari 61 katika shambulio dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini mashariki mwa Somalia katika shambulio lake la jana Alkhamisi. Kambi hiyo ya jeshi ipo katika eneo la jimbo lililojitangazia uhuru wake la Puntland.
Licha ya kuwa, kundi la al Shabab limefurushwa katika miji yote mikubwa na maeneo muhimu ya Somalia, lakini bado wanachama wake katika baadhi ya vijiji na miji hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa Serikali.