Mlipuko wa polio waripotiwa Kongo DR, mikoa 2 yaathiriwa
Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza habari ya mlipuko wa ugonjwa wa kupooza (polio) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ripoti iliyotolewa na WHO jana Jumanne imethibitisha kutokea mlipuko huo katika mikoa ya Haut-Lomami na Maniema, chini ya wiki moja baada ya ugonjwa huo kuripotiwa katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) nchini Syria. Kesi hizi za polio ni mpya kuripotiwa Kongo DR tangu mwaka 2012.
Shirika la Afya Duniani limetoa tathmini inayosema kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kusambaa ugonjwa huo kitaifa DRC na uwezekano wa wastani wa kuenea kimataifa.
Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Shirika la Afya Duniani na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF yalizindua kampeni ya chanjo ya aina yake kuwahi kufanyika katika bara la Afrika dhidi ya polio kwa watoto milioni 116 katika nchi 13 za Afrika Magharibi na Kati.
Nchi hizo 13 ni Benin, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Kodivaa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo , Guinea, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria na Sierra Leone.
Mwaka 1998, jamii ya kimataifa ilipasisha azimio la kuutokomeza ugonjwa wa polio kufikia mwaka 2000 kote duniani, ugonjwa hatari ambao uliwafanya watoto 350,000 kupooza miaka 30 iliyopita, katika nchi 125 kote duniani.