Bunge la Ulaya: Uchunguzi ufanyike kuhusu machafuko mkoani Kasai, Kongo
Bunge la Ulaya limetaka kufanyike uchunguzi kuhusu mauaji na machafuko yanayojiri katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wawakilishi wa Bunge la Ulaya wametoa taarifa wakitaka kuundwe kamisheni ya uchunguzi ya kimataifa kuhusu mauaji na machafuko yaliyoukumba mkoa wa Kasai katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa mauaji hayo.
Wawakilishi wa Bunge la Ulaya wameongeza katika taarifa hiyo kuwa, kamisheni ya uchunguzi itakayoundwa inapasa kuwajumuisha wataalamu wa Umoja wa Mataifa.
Wabunge hao wamebainisha kuwa, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilipasa kuwalinda raia na kutekeleza majukumu yake mkabala na jinai hizo dhidi ya binadamu na za kivita.
Mkoa wa Kasai huko katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekumbwa na mapigano kati ya wanamgambo wanaomuunga mkono Kamwina Nsapu, kiongozi wa kundi la wanamgambo nchini humo na askari usalama wa serikali tangu mwezi Septemba mwaka jana. Watu 3300 wameuawa katika mkoa huo kuanzia mwezi Januari mwaka huu. Makaburi 42 ya umati yamegunduliwa pia huko Kasai.