Kongo DR yaonywa kuhusu hatari ya kuakhirisha uchaguzi
Marais wastaafu wa nchi kadhaa za Kiafrika wameonya juu ya hatari inayoweza kuikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iwapo itaakhirisha uchaguzi wa rais.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, marais wastaafu hao wa nchi kadhaa za Afrika akiwemo Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Olusegun Obasanjo wa Nigeria wametahadharisha kuwa, iwapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakwepa kuitisha uchaguzi kwa mujibu wa katiba, basi kuna hatari ikatumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alimaliza kipindi chake cha pili cha urais mwezi Disemba mwaka jana hata hivyo hakuondoka madarakani kwa madai tofauti.
Muungano tawala huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulifikia makubaliano na vyama vya upinzani kuhusiana na kuitishwa uchaguzi wa rais mwishoni mwa mwakuu huu. Hata hivyo zoezi la kuandikisha wapiga kura limesimama hivi sasa. Hata vyanzo vya kudhamini fedha ya kuitisha uchaguzi huo havijajulikana. Mambo hayo yanapunguza uwezekano wa kufanyika uchaguzi huo mwishoni mwa mwaka huu.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikumbwa na machafuko mwaka jana baada ya Rais Joseph Kabila kuendelea kubakia madarakani licha ya muda wake kumalizika. Makumi ya watu walipoteza maisha kwenye machafuko hayo.