Watu 3300 wameuawa Kasai tangu Oktoba mwaka jana
Duru za habari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimetangaza kuwa, zaidi ya watu elfu tatu wameuawa katika mapigano eneo la Kasai nchini humo.
Duru za habari zimewanukuu viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo wakisema kuwa, jumla ya watu 3300 wameuawa kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa katika mapigano baina ya wanamgambo wanaomuunga mkono Kamwina Nsapu, kiongozi wa kundi la waasi katika eneo hilo la Kasai na askari wa serikali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, askari wamehusishwa na uharibifu wa vijiji 10 katika eneo hilo. Itakumbukwa kuwa tangu mwezi Septemba mwaka jana mji wa Kasai umekuwa ukishuhudia mapigano makali kati ya pande mbili ambapo mbali na maafa makubwa, maelfu ya watu wamelazimika kuwa wakimbizi.
Katika hatua nyingine jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuuawa wanamgambo wa Mai Mai mashariki mwa nchi. Fall Sikabwe, kamanda wa operesheni za kijeshi eneo la mashariki mwa nchi hiyo amesema kuwa, askari watatu wa serikali wamepoteza maisha katika mapigano makali baina ya wanamgambo hao na jeshi. Habari zinasema kuwa, mapigano hayo yalianza Jumatano iliyopita na kwamba wakazi wengi wa eneo la Kabasha kulikojiri mapigano hayo wameyakimbia makazi yao. Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa uwanja wa mapigano tangu miaka 20 iliyopita, kutokana na udhaifu wa jeshi la nchi hiyo katika kuyamaliza makundi ya wanamgambo.