Le Monde: Watoto, wahanga wakuu wa vita vya ndani Congo DR
Gazeti la Le Monde la Ufaransa limeripoti kuwa watoto wadogo katika mji wa Kasai huko katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndiyo wahanga wakuu wa vita katika mji huo.
Gazeti la Le Monde limeandika katika toleo lake la leo kwamba, wanamgambo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaowaondoa kwa mabavu watoto wadogo katika shule za Kasai na kuwaingiza katika mapigano na vita baada ya mafunzo ya miezi kumi.
Le Monde limeandika kuwa, watoto wa Kasai sawa wale wanaotumikishwa kama wanamgambo au raia ndio wahanga wakuu na wa kwanza wa vita na mapigano ya ndani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Limeongeza kuwa, makundi ya wanamgambo huko Congo DR yanawachagua wanachama wao kati ya watoto na watu wenye umri mdogo.
Ripoti iliyotolewa na ofisi ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ya OCHA pia imesema kuwa, watoto wadogo wamekuwa wakisajiliwa na kutumikishwa na makundi ya wanamgambo kutokana na umaskini au woga wa kuuliwa.