Maafisa wa tume ya uchaguzi DRC waliokuwa wametekwa nyara, waachiliwa
Maafisa watatu wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo waliokuwa wametekwa nyara majuma mawili yaliyopita wameachiliwa huru.
Jean-Pierre Mutanda, Naibu Mkuu wa mkoa wa Kasai amesema kuwa, maafisa hao wa Tume Huru ya Uchaguzi waliokuwa wametekwa nyara na wanamgambo ambao ni wafuasi wa kiongozi wa kijadi Kamwina Nsapu aliyeuawa wameachiliwa huru na kwamba, wanatarajiwa kuungana na familia zao masaa machache yajayo.
Mutanda amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Charles Frisby, Mkuu wa Ofisi ya kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MUNUSCO katika mkoa wa Kasai ambapo viongozi hao wamebadilishana mawazo pia kuhusiana na hali ya amani na usalama unaozorota katika nchi hiyo.
Hayo yanajiri huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiendelea kushuhudia harakati za makundi ya waasi hususan mashariki mwa nchi hiyo ambazo zimesababisha mauaji, ukosefu wa amani na raia wengi kuyakimbia makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.
Wakati huo huo, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa jana lilipasisha azimio la kutuma wataalamu wa kimataifa katika eneo la Kasai la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ajili ya kuchunguza mapigano na machafuko yaliyotokea katika mji huo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu milioni 1.3 wameyakimbia makazi yao katika eneo hilo la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na machafuko hayo.