Jun 25, 2017 03:44 UTC
  • Serikali ya Mali yaanza mazungumzo na waasi

Serikali ya Mali imetangaza kuwa, mazungumzo ya amani kati yake na makundi ya waasi yaliyokwama mwaka 2015 yameanza tena .

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mazungumzo hayo yenye lengo la kurejesha amani katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inayotaabika kwa ukosefu wa usalama yalianza tena hapo jana Jumamosi.

Mbunge mmoja wa Bunge la Mali amewaambia waandishi wa habari mjini Bamako kwamba, licha ya kuwa huko nyuma serikali ya nchi hiyo ilikuwa imetiliana saini makubaliano ya amani na makaundi ya waasi, lakini makubaliano hayo yalivurugika kutokana na waasi kujiunga na makundi ya kigaidi.

Kuanza tena kwa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Mali na makundi ya waasi kumepongezwa na duru mbalimbali hasa katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa usalama.

Waasi wa kaskazini mwa Mali

Mali imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha licha ya kuweko askari wa kimataifa wa kulinda amani nchini humo.  

Ilikuwa nchi yenye utulivu, lakini mwaka 2012 wanajeshi walifanya mapinduzi na baada ya hapo kukazuka makundi ya watu wenye silaha walioteka maeneo kadhaa ya kaskazini mwa nchi hiyo kabla ya kufurushwa kwenye baadhi ya maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kwa sasa karibu moja ya tano ya wananchi wa Mali wanahitajia misaada ya haraka ya kibinadamu na inatabiriwa kuwa, katika miezi michache ijayo raia milioni nne wa nchi hiyo watakabiliwa na hatari ya ukosefu wa chakula.

 

 

 

 

 

 

Tags