Wabunge wa DRC waitaka serikali kuimarisha usalama nchini mwao
Wawakilishi kadhaa wa bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutoka maeneo tofauti ya nchi hiyo, wametaka kuongezwa hatua za kiusalama ndani ya baadhi ya miji hususan ya mashariki.
Jérôme Lusenge, Msemaji wa Baraza la Wawakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameitaka serikali ya nchi hiyo kuongeza hatua za usalama katika mji wa Beni, kaskazini magharibi mwa taifa hilo, kufuatia mashambulizi ya siku ya Alkhamis iliyopita ya waasi wa Mai Mai katika mji huo.
Hii ni katika hali ambayo serikali ilituma askari kadhaa katika maeneo ya Lubero na Butembe mjini Beni baada ya kujiri hujuma hizo za waasi. Baadhi ya duru za habari mjini hapo zimetangaza kuwa, askari wa serikali walipata taarifa ya kutokea shambulizi hilo kupitia asasi za kiraia katika eneo, lakini hata hivyo hawakuchukua hatua yoyote ya kuzuia hujuma hiyo. Inaelezwa kuwa akthari ya waasi waliohusika na shambulizi hilo ni wafungwa waliotoroka kutoka jela kuu ya mji wa Beni.
Vitendo vya utumiaji mabavu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vilianza kushika kasi katika wiki iliyopita kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea kushuhudiwa nchini.