Makaburi mengine ya umati yagunduliwa Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31010-makaburi_mengine_ya_umati_yagunduliwa_kasai_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo
Serikali yai Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa, imegundua zaidi ya makaburi kumi ya umati katika mkoa wa Kasai, mahali ambapo vikosi vya serikali na makundi ya waasi yametuhumiwa kwa kufanya mauaji dhidi ya raia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 26, 2017 23:25 UTC
  • Makaburi mengine ya umati yagunduliwa Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Serikali yai Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa, imegundua zaidi ya makaburi kumi ya umati katika mkoa wa Kasai, mahali ambapo vikosi vya serikali na makundi ya waasi yametuhumiwa kwa kufanya mauaji dhidi ya raia.

Meja Jenerali, Joseph Ponde Mwendesha Mastaka wa kijeshi amesema kuwa, anaamini mauaji hayo yamefanywa na baadhi ya waasi wa aliyekuwa kiongozi wa kijadi Kamwina Nsapu ambao wamekuwa wakuiendesha mapigano dhidi ya serikali tangu kiongozi wao huyo alipouawa.

Hii si mara ya kwanza katika kipindi cha majuma machache yaliyopita, kugunduliwa makaburi ya umati katika mkoa wa Kasai. Makumi ya makaburi mengine ya umati yamegunduliwa hivi karibuni katika mkoa huo na kuongeza wasiwasi wa kuweko ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika katika maeneo hayo.

kasai

Baadhi ya maiti zilizopatikana katika makaburi ya umati mkoani Kasai

Watu zaidi ya 3,300 wameuawa katika miezi michaache baada ya kuongezeka kwa machafuko katika mkoa wa Kasai katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa ulisema kuwa, utatuma timu ya wataalamu kuchunguza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mkoa huo.

Eneo la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekumbwa na machafuko ya umwagaji wa damu tangu mwezi Septemba 2016 na tangu wakati huo hadi hivi sasa, vikosi vya serikali vinapambana na kundi moja la waasi lililozuka kwenye eneo hilo.