Save the Children: Maelfu ya watoto Somalia watakufa kwa njaa
Taasisi moja ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu imetahadharisha kuhusu hatari ya kuaga dunia watoto wa Kisomali elfu 20 kutokana na ukame na njaa iliyoiathiri Somalia.
Hassan Noor Saadi, Mkurugenzi wa taasisi ya Save the Children nchini Somalia amesema kuwa watoto elfu 20 wataaga dunia kwa njaa kali huko Somalia iwapo misaada ya kibinadamu haitapelekwa nchini humo.
Ripoti iliyotolewa na Save the Children imeeleza kuwa, lishe duni inatishia maisha ya nusu ya watoto katika maeneo tisa ya Somalia yaliyokumbwa na ukame.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo nchini Somalia amebainisha kuwa, mvua zilizonyesha hivi karibuni hazikuwa za kutosha na kwamba hazikuwa na taathira katika uzalishaji wa mazao jambo ambalo limezidisha wasiwasi kuhusu akiba ya chakula nchini Somalia.
Hassan Noor Saadi ameongeza kuwa, kiasi cha karibu dola bilioni moja na nusu kinahitajika kwa ajili ya kukabiliana na baa la njaa huko Somalia na kwamba, hadi kufikia sasa kumetengwa bajeti ya dola milioni 550 tu katika uwanja huo.
Umoja wa Mataifa pia umetangaza kuwa, watu milioni sita na laki saba wanahitaji misaada ya dharura ya kibinadamu huko Somalia na kwamba hali ya mambo inazidi kuwa mbaya.