Watu watatu wauawa katika hujuma ya kigaidi msikitini Cameroon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31200-watu_watatu_wauawa_katika_hujuma_ya_kigaidi_msikitini_cameroon
Magaidi wajirupua nje ya msikiti nchini Cameroon na kuwaua watu watatu Ijumaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2017 08:54 UTC
  • Watu watatu wauawa katika hujuma ya kigaidi msikitini Cameroon

Magaidi wajirupua nje ya msikiti nchini Cameroon na kuwaua watu watatu Ijumaa.

Taarifa zinasema kuwa, magaidi wa kike waliokuwa wamejifunga mishipi ya mabomu walijiripua katika mlango wa msikiti mjini Kerawa kaskazini mwa Cameroon.

Maafisa wa usalama wanasema, vijana wanaolinda msikiti huo waliwatambua magaidi waliokuwa wamefika eneo hilo wakati wa Swala ya Alfajiri. Baada ya magaidi kugundua kuwa wameshatambuliwa, walijilipua na kuua waumini watatu waliokuwa wamefika msikitini hapo kuswali.

Wakuu wa usalama nchini Cameroon wanasema hujuma hiyo imetekelezwa na magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram ambao sasa imekuwa ada yao kufanya hujuma za kigaidi kila Ijumaa eneo hilo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Cameroon, baina ya mwezi Januari na Juni mwaka huu wa 2017, watu takribani 20 wameuawa katika hujuma za Boko Haram. Aidha kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 26 katika Ukanda wa Ziwa Chad unaojumuisha nchi za Nigeria, Cameroon, Chad na Niger wanakabiliwa na hatari ya hujuma za magaidi wa Boko Haram. Ugaidi huo umesababisha watu milioni 2.6 katika eneo hilo kuwa wakimbizi.

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu elfu 20 wamepoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria na eneo la Ukanda wa Ziwa Chad.