Al Shabab waua Polisi 2 katika hujuma huko Lamu, Kenya
Maafisa wawili wa polisi nchini Kenya wameuawa baada ya magaidi wanaoaminika kuwa wa kundi la Al Shabab kushambulia kituo cha polisi katika eneo la Pandanguo katika Kaunti ya Lamu.
Taarifa zinasema maafisa wengine saba wa polisi hawajulikani waliko baada ya magaidi wanaokadiriwa kuwa 200 kushambulia kituo kidogo cha polisi cha Pandanguo.
Duru zinadokeza kuwa, magaidi hao walishamulia kituo hicho mapema leo Alfajiri baada ya kuswali katika msikiti ulio karibu. Katika makabiliano na maafisa wa polisi, magaidi wawili pia wanaripotiwa kuuawa.
Tukio hilo linakuja wiki mbili baada ya watu 8 wakiwemo maafisa wanne wa polisi na wanafunzi wanne kupoteza maisha baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini mashariki mwa Lamu. Maafisa wa usalama wanasema, bomu hilo lilikuwa limetegwa na magaidi wa Al Shabab.
Ingawa kundi la Al Shabab halijatangaza kuhusika na hujuma hizo, lakini inaaminika watu wanaofungamana na kundi hilo la magaidi wakufurishaji ndio wanaotekeleza mauaji hayo. Hivi karibuni Mratibu wa Serikali katika Kanda ya Pwani, Nelson Marwa alisema serikali itatekeleza oparesheni kali ya kuwatimua magaidi kutoka maficho yao katika msitu wa Boni huko Lamu.