Marekani yafanya njama za kujipenyeza zaidi nchini Libya
Serikali ya Libya imetangaza kuwa itaongeza idadi ya wanajeshi wake nchini Libya
Televisheni ya CNN imewanukuu maafisa wa serikali ya Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao wakisema kuwa, serikali ya Donald Trump ina mkakati wa kujiimarisha kijeshi na kisiasa nchini Libya.
Kwa mujibu wa televisheni hiyo, siasa mpya za Marekani nchini Libya zinatarajiwa kuishia kwenye kufungua upya ubalozi wa nchi hiyo mjini Tripoli.
Maafisa hao wa serikali ya Marekani wameongeza kuwa, hivi sasa Washington inachunguza njia za kufungua ubalozi wake mdogo katika mji wa Benghazi Libya. Ubalozi mdogo wa Marekani ulifungwa mjini Benghazi baada ya kuuliwa wafanyakazi kadhaa wa ubalozi huo mwaka 2012
Hadi leo hii Libya imeshindwa kuwa salama tangu Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ulipoivamia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kufanya mauaji makubwa pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu kwa madai ya kumpindua Kanali Muammar Gaddafi na baadaye kuitelekeza huku silaha za kila namna zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi tofauti mwaka 2011 .
Uingiliaji wa madola ya kigeni ya kieneo na kimataifa ndio unaolaumiwa kwa kushadidisha mgogoro nchini Libya kiasi kwamba juhudi zote za kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo zimekuwa zikikwama.
Ni hivi karibuni tu ambapo Ahmed al Mismari, msemaji wa wapiganaji wa serikali yenye makao yake huko mashariki mwa Libya alisema mwanzoni mwa mwaka huu kwamba, Uturuki ndiye muungaji mkono mkubwa wa makundi ya kigaidi nchini humo.