Makaburi mengine 38 ya umati yagunduliwa Congo DR
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, umegundua makaburi mengine 38 ya umati katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ofisi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, makaburi hayo ya umati yamegunduliwa katika maeneo sita tofauti katika operesheni ya pamoja na maafisa wa uchunguzi wa jeshi la Congo katika eneo la magharibi mwa Kasai.
Kwa utaratibu huo idadi ya makaburi ya umati yaliyogunduliwa hadi sasa nchini Congo tangu waasi wa mashariki mwa nchi hiyo waanze harakati zao katika eneo hilo mwezi Agosti mwaka jana imefikia makaburi zaidi ya 80.
Zaidi ya watu elfu tatu na mia tatu (3300) wameuawa na wengine milioni moja na laki nne wamelazimika kukimbia makazi yao katika eneo la Kasai kutokana na machafuko hayo.
Maeneo ya Mashariki mwa Congo yanasumbuliwa na machafuko makubwa kwa miaka kadhaa sasa.