Kuongezeka idadi ya wahitaji wa misaada ya chakula barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i3178-kuongezeka_idadi_ya_wahitaji_wa_misaada_ya_chakula_barani_afrika
Kiongozi mmoja wa serikali ya Zimbabwe, ameelezea ongezeko kubwa la wahitaji wa misaada ya chakula kutokana na kushadidi ukame nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 16, 2016 10:26 UTC
  • Kuongezeka idadi ya wahitaji wa misaada ya chakula barani Afrika

Kiongozi mmoja wa serikali ya Zimbabwe, ameelezea ongezeko kubwa la wahitaji wa misaada ya chakula kutokana na kushadidi ukame nchini humo.

Prisca Mupfumira, Waziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii nchini Zimbabwe ametangaza kuwa, idadi ya watu wanaohitaji chakula imepindukia na kufikia milioni nne. Kabla ya hapo Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe alinukuliwa akisema kuwa, serikali ya Harare inahitajia kiasi cha dola bilioni moja na nusu kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo kati ya mwezi Februari hadi Disemba mwaka huu. Mnangagwa amesema, serikali inahitajika kuingiza nchini humo kiwango cha tani milioni moja na nusu za mahindi kwa ajili ya wananchi. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, katika hali ambayo Zimbabwe ilikuwa ikijulikana kama ghala la chakula la Afrika, hivi sasa si tu kwamba ukame mkali umemaliza kabisa chakula nchini humo, bali hata mvua zinazonyesha kwa ajili ya kudhamini maji yanayohitajika majumbani pia hazitoshi. Kadhalika wanyamapori nao wameathirika sana na hali hiyo na kufanya idadi kubwa ya wanyama hao kufariki dunia. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aliielezea hali mbaya ya ukosefu wa chakula nchini kwake kuwa ni janga la kitaifa. Aidha Rais Mugabe amewataka viongozi wa serikali, mashirika na taasisi za kujitolea, kuwasaidia wananchi kukabiliana na tatizo hilo la njaa nchini. Hali ya tabianchi ijulikanayo kama El Nino si tu kwamba imeisababishia nchi hiyo ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita, bali imeathiri pia hata nchi nyingine za Kiafrika. Kufuatia hali hiyo, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Watoto (UNICEF) umetangaza kuwa hali ya tabianchi ya El Nino imewasababishia hali mbaya karibu watoto milioni moja wa mashariki na kusini mwa bara la Afrika kutokana na uhaba mkubwa wa chakula, huku eneo lililoathirika zaidi likiwa ni la kusini mwa bara hilo, hadi kutangazwa hali ya hatari. Nchini Ethiopia pia imetangazwa kuwa, kati ya raia milioni 10 hadi 18 wa nchi hiyo wanahitaji msaada wa haraka wa chakula katika kipindi cha mwaka huu. Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya Afrika Kusini, kupungua kwa mvua, kumeisababishia sekta ya kilimo nchini humoo matatizo makubwa . Aidha serikali ya Pretoria imetangaza kupata hasara ya kiasi cha dola bilioni moja mwaka jana katika sekta ya kilimo kutokana na ukame mkubwa. Kufuatia ukame huo, serikali ya nchi hiyo imelazimika kuagiza kwa akali tani milioni nne za mahindi ili kukabiliana na hali mbaya ya ukosefu wa chakula. Mbali na nchi hizo, ukame unashuhudiwa pia katika nchi kadhaa za Kiafrika kama vile Sudan Kusini na Malawi. Hii ni katika hali ambayo Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo FAO limetabiri kuendelea kupungua kiwango cha mvua zinazonyesha barani Afrika, suala ambalo litafanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi.