Siasa mpya za Trump ni kuingilia zaidi masuala ya ndani ya Libya
Gazeti la al Quds al Arabi limeandika kuwa, serikali ya Donald Trump ya nchini Marekani inatumia kisingizio cha makundi ya kigaidi kuingilia masuala ya ndani ya Libya.
Gazeti hilo linalochapishwa mjini London Uingereza liliandika jana (Jumapili) kuwa, Marekani imeamua kufuata siasa za kuingilia zaidi masuala ya ndani ya Libya kwa madai ya kupambana na magenge ya kigaidi, kuzuia kile kinachodaiwa kuwa ni ushawishi wa Russia nchini Libya na hali mbaya ya ukosefu wa amani na usalama katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, inavyoonekana siasa mpya za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine zitaanza kutekelezwa wiki kadhaa zijazo kwa lengo la kufanikisha malengo ya Washington nchini Libya.
Hatua ya Marekani ya kuanzisha tena mashambulizi makubwa ya anga tena kwa namna tofauti kabisa na huko nyuma imezusha maswali mengi kuhusu nafasi ambayo Washington inakusudia kuichukua karibuni hivi nchini Libya.
Hadi hivi sasa Libya haijawahi kushuhudia utulivu na amani ya aina yoyote ile tangu Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO lilipoingilia masuala ya ndani ya Libya mwaka 2011 na kufanya uharibifu mkubwa hasa wa miundombinu kwa madai ya kumpindua Kanali Muammar Gaddafi na baadaye kuhakikisha linaaacha silaha za kila namna zikiwa zimezagaa mikononi mwa watu na makundi mengi hasimu nchini humo.
Uingiliaji wa kigeni wa madola ya kieneo na kimataifa katika masuala ya ndani ya Libya ndio unaolaumiwa kwa kukwamisha juhudi zote za kuitafutia ufumbuzi migogoro ya nchi hiyo.