Haftar asisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya magaidi
Khalifa Haftar Kamanda wa jeshi la taifa la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo amesema kuwa mapambano dhidi ya ugaidi hadi kutokomezwa suala hilo yataendelezwa kote nchini Libya.
Kamanda Haftar amesema kuwa bado kuna safari ndefu na ngumu hadi kufikia ushindi wa mwisho mbele ya magaidi huko Libya na kwamba vita kati yao na magaidi bado havijamalizika. Jenerali Khalifa Haftar amesema kuwa vyanzo vya kiuchumi na mapato kwa magaidi vinapasa kusitishwa ili kuweza kuwatokomeza magaidi hao. Mji wa Benghazi tangu miaka mitatu iliyopita hadi sasa umekumbwa na mapigano kati ya jeshi la taifa la Libya na wanamgambo wa Baraza la Mapinduzi ya Benghazi ambao wana uhusiano wa karibu na kundi la kigaidi la Daesh.
Jenerali Khalifa Haftar tarehe 5 mwezi huu alitangaza kuwa vikosi vya jeshi la Libya vinaudhibiti kikamilifu mji wa Benghazi baada ya miaka mitatu ya vita vya umwagaji damu, hata hivyo mapigano yangali yanaendelea katika baadhi ya maeneo ya mji huo kati ya vikosi vya Libya na magaidi. Libya ilitumbukia katika machafuko ya kisiasa na hali ya mchafukoge baada ya kupinduliwa madarakani dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 na kufuatia uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo.