UN: Kuna uwezekano waasi na vyombo vya usalama viliwaua watumishi wetu
Kundi moja la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa, kuna uwezekano makundi ya wababe silaha na maafisa wa vyombo vya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, walihusika katika mauaji dhidi ya wataalamu wa umoja huo waliokuwa wakichunguza kuhusu makaburi ya umati nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo la UN imesema kuwa, nyaraka zilizopatikana zinaonyesha kwamba, wahusika wa jinai hiyo dhidi ya Zida Catalan, raia wa Sweden na Michael Sharp raia wa Marekani, ni watu tofauti kama vile wanamgambo wanaomuunga mkono Kamwina Nsapu, kiongozi wa kundi la waasi wa kikabila, makundi mengine ya wabeba silaha na pia wahusika wa vyombo vya usalama nchini humo.
Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa waliuawa tarehe 12 Machi mwaka huu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kundi hilo la Umoja wa Mataifa limesema kuwa, baada ya kuchunguza mawasiliano ya simu yaliyorekodiwa kuhusiana na suala la mauaji ya watu hao, imeonekana kuwa kabla ya wataalamu hao wa UN kuuawa walienda kufanya mazungumzo na mmoja wa viongozi wa kabila la Kamwina Nsapu na kwamba mauaji dhidi yao yalitokea muda punde baada ya mazungumzo hayo.
Zida Catalan na Michael Sharp walitumwa na António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenda mkoa wa Kasai, katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuchunguza sababu za machafuko yanayoendelea katika mkoa huo.