Ofisa wa Umoja wa Mataifa ataka amani irudi Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32092-ofisa_wa_umoja_wa_mataifa_ataka_amani_irudi_sudan_kusini
Msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ulinzi wa amani El Ghassim Wane amesema changamoto zinazoikabili Sudan Kusini zinatakiwa kuondolewa, ili kutumia fursa ya uwepo wa vikosi vya ulinzi wa usalama kuirudisha nchi hiyo kwenye hali ya utulivu na usalama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2017 22:02 UTC
  • Ofisa wa Umoja wa Mataifa ataka amani irudi Sudan Kusini

Msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ulinzi wa amani El Ghassim Wane amesema changamoto zinazoikabili Sudan Kusini zinatakiwa kuondolewa, ili kutumia fursa ya uwepo wa vikosi vya ulinzi wa usalama kuirudisha nchi hiyo kwenye hali ya utulivu na usalama.

Wane ameonya kuwa kwa sasa hali ya usalama bado ni dhaifu, na kusema Sudan Kusini inahitaji usimamishaji vita halisi na wenye kuaminika. Ameongeza kuwa kila juhudi inatakiwa kufanywa kuhakikisha kuwa "mjadala wa kitaifa" unakuwa shirikishi, wazi na unafanyika katika mazingira huru na salama, na kuungwa mkono kwa maafikiano makubwa ya kisiasa. Pia ameitaka jumuiya ya kimataifa kuifahamisha serikali ya Sudan Kusini kuwa hali ya sasa haikuibaliki na si ya kudumu.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa  Sudan Kusini

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Hivi sasa Machar yuko uhamishoni nchini Afrika Kusini huku nchi hiyo changa zaidi duniani ikiendelea kushuhudia mapigano baina ya vikosi vya serikali na waasi na hivyo kupelekea makumi ya maelfu ya watu kukimbilia usalama katika nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa za kupatanisha pande hasimu hadi sasa hazijazaa matunda.