Askari wa Khalifa Haftar wamewaua wafungwa 20
Askari wa Khalifa Haftar, kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya wamewaua wafungwa 20 kwa tuhuma za kuhusika na kuteka nyara na kutesa askari wa kamanda huyo.
Mkanda wa video uliosambaa unaowanyesha askari wa Khalifa Haftar wakiwamiminia risasi wafungwa hao 20 waliokuwa wamefungwa vitambaa usoni na kuvishwa mavazi ya rangi ya njano, tukio ambalo lilishabihiana sana na jinai zinazofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS).
Baada ya askari hao kusikia amri ya kupiga risasi kutoka kwa Mahmoud Warfali, mmoja wa viongozi wa juu wa jeshi la taifa, walianza kuwamiminia risasi wafungwa hao. Hii ni katika hali ambayo Jumanne iliyopita Umoja wa Mataifa uliwataka makamanda wa jeshi nchini Libya kumtimua jeshini Mahmoud Warfali na kuanzisha uchunguzi wa faili la kuhusika kwake na vitendo vya utesaji na kuua mateka bila kuwafikisha mahakamani.
Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa, kuna uwezekano wa kukaririwa jinai hizo iwapo wahusika hawatochukuliwa hatua kali za kisheria.
Libya ilitumbukia katika machafuko tangu mwaka 2011 kufuatia mashambulizi ya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) yaliyopelekea kuondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.