Maiti 13 za wahajiri zapatikana katika boti ya plastiki Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32254-maiti_13_za_wahajiri_zapatikana_katika_boti_ya_plastiki_libya
Miili 13 ya wahajiri waliokuwa wakielekea barani Ulaya imepatikana ndani ya boti ya plastiki na wapiga mbizi wa shirika moja lisilo la serikali katika pwani ya Libya.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jul 25, 2017 12:00 UTC
  • Maiti 13 za wahajiri zapatikana katika boti ya plastiki Libya

Miili 13 ya wahajiri waliokuwa wakielekea barani Ulaya imepatikana ndani ya boti ya plastiki na wapiga mbizi wa shirika moja lisilo la serikali katika pwani ya Libya.

Muasisi wa shiriki hilo linaloitwa Proactiva Open Arms amesema miili hiyo imepatikana na wahudumu wa asasi hiyo ya kijamii ndani ya boti ya plastiki iliyokuwa imebeba wahajiri zaidi ya 160.

Oscar Camps ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, "Miili ya wanawake wajawazito ni miongoni mwa maiti hizo zilizopatikana karibu na pwani ya Libya.

Haya yanajiri katika hali ambayo, mapema leo Gadi ya Pwani ya Libya imetangaza habari ya kuokolewa wahajiri haramu 300 karibu na miji ya Zawiya na Sabratha katika maji ya pwani ya magharibi mwa mji mkuu Tripol. Wahajiri wengine 600 waliokolewa jana baada ya boti zao kuzama kusini mwa bahari ya Mediterrania.

Wahajiri wa Kiafrika wakielekea Ulaya kupitia bahari ya ya Mediterrania 

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, karibu wahajiri elfu mbili wamepoteza maisha yao ndani ya bahari ya Mediterrania, wakiwa katika safari hatari za kuelekea Ulaya kutafuta ajira na maisha bora.

Kwa mujibu wa Shirika la Wahajiri Duniani IOM, wahajiri zaidi ya elfu tano aghlabau wakiwa raia wa nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia walifariki dunia kwa kuzama katika bahari ya Mediterrania wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya.