Kurejea kwa Seiful Islam katika ulingo wa siasa Libya, kifo cha uadilifu
Kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya, Jenerali Khalifa Haftar ametoa matamshi ya kustaajabisha pale alipodai kuwa, mwana wa dikteta wa zamani wa Libya, Seiful Islam Gaddafi anaweza kuwa na nafasi katika mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo.
Jenerali Haftar ameliambia gazeti la al Hayat kuwa, Seiful Islam ni raia wa kawaida wa Libya na kwamba hana tatizo binafsi na yeye bali anamkaribisha. Haftar ameongeza kuwa: Seiful Islam anaweza kuwa na nafasi katika siasa za Libya.
Libya ilikuwa nchi ya tatu baada ya Tunisia na Misri kukumbwa na wimbi la mapinduzi ya wananchi lililoziondoa madarakani tawala za kidikteta za nchi hizo. Tofauti kubwa zaidi baina ya mapinduzi ya Libya na yale ya nchi kama Misri na Tunisia ni kwamba, Muammar Gaddafi aliingiza Libya katika vita vya ndani vilivyoendelea kwa kipindi cha miezi 9 na hatimaye utawala wake wa kidikteta ulipinduliwa baada ya kiongozi wake kuuliwa. Kwa msingi huo watu wa Libya - hata kabla ya wenzao wa Tunisia na Misri- walitaka kutekelezwa uadilifu wa baada ya machafuko (Transitional Justice) kuhusu viongozi wa zamani wa nchi hiyo. Uadilifu wa aina hiyo hupata maana katika jamii ambazo zilikuwa na tawala za kidikteta na hakukuwepo uwezekano wa kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wahalifu katika tawala hizo, na baada ya kuporomoka tawala hizo za kidikteta na kuja madarakani utawala mpya, suala la kutekelezwa uadilifu huwa miongoni mwa matakwa muhimu na makuu ya watu katika nchi na jamii hizo.
Serikali za mpito au za muda zilizoshika madaraka baada ya Gaddafi nchini Libya zilielewa vyema matakwa ya wananchi ya kutaka kutekelezwa uadilifu dhidi ya viongozi wa zamani wa nchi hiyo lakini zilichukua hatua pungufu na na zisizokuwa kamili katika uwanja huo kama vile kuunda kamisheni ya kutafuta ukweli na kuwafikisha mahakamani viongozi wa zamani wa nchi hiyo. Vilevile Bunge la Libya likishirikiana na Wizara ya Sheria ya serikali ya mpito ya nchi hiyo limepasisha sheria ya kutoa msamaha kwa baadhi ya viongozi wa utawala wa zamani wa nchi hiyo, hatua ambayo pia ni miongoni mwa taratibu za kile kinachojulikana kama Transitional Justice. Hata hivyo sheria ya Bunge la Libya imetaka kupewa msamaha maafisa wa serikali ya zamani ambao hawakutenda jinai dhidi ya raia.
Pamoja na hayo inaonekana kuwa, Jenerali Khalifa Haftar, jeshi lake, baadhi ya makundi na wanasiasa wenye ushawishi nchini Libya wanataka pia kutekelezwa sharia hiyo ya msamaha kwa Seiful Islam Gaddafi. Katika mkondo huo jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali huyo mwezi Juni mwaka huu lilimuachia huru Seiful Islamu Gaddaf kwa madai kuwa limetekeleza amri ya Wizara ya Sheria ya serikali ya mpito.
Ukweli ni kuwa, kuachiwa huru Seiful Islam Gaddafi kunatokomeza kabisa matumaini kiduchu ya wananchi wa Libya ya kutaka kuona haki na uadilifu ukitekelezwa. Hii ni kwa sababu Seiful Islamu, mwana wa dikteta wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi alikuwa na nafasi kubwa katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika katika kipindi cha miongo minne cha utawala wa baba yake nchini Libya. Si hayo tu bali Seiful Islam alikuwa nguzo kuu ya kuchukua maamuzi katika vita vya miezi tisa vya ndani ambavyo vimeua maelfu ya watu na kujeruhiwe wengine wengi.
Suala la mwisho linalopaswa kuashiriwa hapa ni kuwa, matamshi ya Jenerali Khalifa Haftar yametolewa baada ya kukutana na hasimu wake, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa, Fayez al Sarraj Jumanne iliyopita nchini Ufaransa na kutia saini makubaliano ya Paris, na kwa msingi huo inaonekana kuwa, matamshi hayo ya Haftar yana mfungamano kwa njia moja au nyingine na makubaliano hayo ya Paris.