Serikali ya maridhiano ya kitaifa Libya yakaribisha kupitishwa rasimu ya katiba
Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya maridhiano ya kitaifa ya Libya amekaribisha kupitishwa rasimu ya katiba mpya na Baraza la Kutunga Katiba la nchi hiyo na kutoa wito wa kuitishwa kura ya maoni ya kupitisha rasmi katiba hiyo.
Katika taarifa aliyotoa kuhusiana na suala hilo, Al-Sarraj aidha amewataka maafisa husika kuandaa mazingira mwafaka kwa ajili ya kufanyika kura ya maoni ya kuamua kuhusu rasimu hiyo.
Katika kikao chake kilichofanyika katika mji wa Al-Baydhaa, Baraza la Kutunga Katiba la Libya limeipitisha rasimu ya katiba hiyo kwa kura 43 kati ya 44 za wajumbe wote wa baraza hilo.
Kwa muda wa miaka 40 Libya ilikuwa chini ya utawala wa Muammar Gaddafi, na haijawa na katiba kwa muda wote tangu ulipoangushwa utawala wake mwaka 2011.
Katiba mpya ya Libya itakuwa na vifungu 197.
Kwa mujibu wa rasimu ya katiba hiyo, Libya itakuwa nchi ya Jamhuri, yenye Rais, Bunge na Baraza la Seneti na Tripoli ukiwa ndio mji wake mkuu. Aidha Uislamu unatambuliwa kama dini rasmi ya nchi hiyo na dini, itakuwa moja ya marejeo ya kutunga sheria za nchi.
Katiba mpya ya Libya, aidha inazitambua lugha nne za Kiarabu, Kiamazighi, Kituareg na Kitabawi kuwa lugha rasmi za nchi hiyo.
Libya imekuwa ikishuhudia machafuko na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa tangu baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011 yaliyohitimisha miaka 40 ya utawala wa Gaddafi kutokana na uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo.
Aidha kutokana na hitilafu za vyama na makundi ya kisiasa, tangu miaka miwili nyuma, nchi hiyo imekuwa ikiongozwa na mabunge mawili kwa wakati mmoja, moja likiwa na makao yake katika mji wa Tabruk na jengine katika mji mkuu Tripoli pamoja na majeshi mawili tofauti.../