Jeshi la Cameroon laangamiza Boko Haram 20 nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i3259-jeshi_la_cameroon_laangamiza_boko_haram_20_nchini_nigeria
Wanajeshi wa Cameroon wametangaza kuangamiza wanachama 20 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika operesheni iliyofanyika huko kaskazini mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2016 10:33 UTC
  • Jeshi la Cameroon laangamiza Boko Haram 20 nchini Nigeria

Wanajeshi wa Cameroon wametangaza kuangamiza wanachama 20 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika operesheni iliyofanyika huko kaskazini mwa Nigeria.

Kanali Jacob Kodji, kamanda mwandamizi wa jeshi la Cameroon amesema kuwa, operesheni hiyo ya jana Jumatano ya kuwaangamiza wanamgambo wa Boko Haram ilifanyika katika mji wa Djibrila, yapata kilomita 10 kutoka mpaka wa Cameroon. Naye Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Cameroon, Kanali Didier Badjeck amesema mateka 12 wameokolewa kutoka mikononi mwa magaidi hao sambamba na kupata silaha na magari ya kijeshi yaliyokuwa yameibiwa na matakfiri wa Boko Haram. Operesheni ya Jumatano dhidi ya Boko Haram imefanyika siku moja baada ya wanachama wa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri kuua watu 22 waliokuwa wakisali katika msikiti wa jimbo la Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Benin imesema kuwa, mwezi ujao nchi hiyo itatuma kikosi cha askari 150 watakaojiunga na kile kinachoundwa na nchi kadhaa ambacho kimekuwa kikikabiliana na wanamgambo wa Boko Haram ambao wamehatarisha usalama katika nchi ya Nigeria na katika mipaka ya nchi nyengine ikiwemo Cameroon. Inadaiwa kuwa kuna wanamgambo 8700 wa Boko Haram kwenye eneo hilo. Watu zaidi ya 20,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni 2.5 wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi tangu kundi la Boko Haram lianzishe hujuma zake nchini Nigeria mwaka 2009.