Niger yatoa mwito kwa jamii ya kimataifa kusaidia mapambano dhidi ya ugaidi
Rais wa Niger ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa akitaka kuungwa mkono haraka iwezekanavyo mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Sahel barani Afrika. Rais wa Niger ametoa ombi hilo katika maadhimisho ya mwaka 57 wa uhuru wa nchi hiyo.
Rais Mahamaduo Issoufou wa Niger jana alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuimarisha na kukipatia zana za kijeshi kikosi cha pamoja cha G-5 cha Sahel kinachotekeleza oparesheni dhidi ya makundi yenye misimamo mikali na yale ya kigaidi katika eneo hilo. Rais wa Niger ametaka pia nchi za eneo la Sahel zipatiwe vyanzo vya kifedha vinavyohitajika ili kufikia malengo ya kikosi hicho. Kundi la G-5 liliundwa mwaka 2014 na linajumuisha wanajeshi kutoka Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger na Chad.
Tarehe Sita mwezi Februari mwaka huu kundi hilo lilipasisha azimio na kuamua kuasisi kikosi cha pamoja na wanajeshi kutoka nchi hizo kwa ajili ya kukabiliana na ukosefu wa amani, makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na ugaidi katika eneo la Sahel barani Afrika. Eneo la Sahel linaundwa na maeneo kuanzia magharibi hadi masharki yaani eneo la kaskazini mwa Senegal, kusini mwa Mauritania, katikati mwa Mali, kusini mwa Algeria na Niger, katikati mwa Chad, kusini mwa Sudan, kaskazini mwa Sudan Kusini na Eritrea.