UNICEF: Watoto nusu milioni wa Libya wanahitaji msaada wa dharura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32992-unicef_watoto_nusu_milioni_wa_libya_wanahitaji_msaada_wa_dharura
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema watoto zaidi ya laki tano nchini Libya wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na mapigano ya pande hasimu za kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 11, 2017 02:48 UTC
  • UNICEF: Watoto nusu milioni wa Libya wanahitaji msaada wa dharura

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema watoto zaidi ya laki tano nchini Libya wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na mapigano ya pande hasimu za kisiasa nchini humo.

Geert Cappelaere, Mkurugenzi wa kieneo wa UNICEF amesema watoto 550,000 wanahitajia msaada wa dharura wa kibinadamu na kusisitiza kuwa wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Ameongeza kuwa, mgogoro huo mbali na kuvuruga uchumi wa taifa umefanya aghalabu ya watoto wakimbie makazi yao na kuishia katika kambi za wakimbizi.

Kadhalika afisa huyo wa UN amezitaka pande hasimu za kisiasa nchini Libya kusitisha mapigano na kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo haraka iwezekanavyo. 

Mtoto akijaribu kujifunza nje baada ya shule yao kusambaratishwa

Libya imekuwa ikishuhudia machafuko na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa tangu baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011 yaliyohitimisha miaka 40 ya utawala wa Kanali Muammar Gaddafi kutokana na uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo.

Aidha kutokana na hitilafu za vyama na makundi ya kisiasa, tangu miaka miwili nyuma, nchi hiyo imekuwa ikiongozwa na mabunge mawili kwa wakati mmoja, moja likiwa na makao yake katika mji wa Tobruk na jengine katika mji mkuu Tripoli pamoja na majeshi mawili tofauti.

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kuwa, watoto zaidi ya 80 elfu wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani, laki mbili wanahitaji maji safi ya kunywa, huku laki 5 na elfu 50 wakikatiza masomo baada ya shule zaidi ya 550 nchini humo kuharibiwa au zinatumika kama hifadhi ya wakimbizi.