Uganda yakadhibisha kutuma wanajeshi wake huko Kenya
Serikali ya Uganda imekadhibisha madai kuwa ina nia ya kutuma wanajeshi wake huko Kenya ili kusaidia polisi wa nchi hiyo katika oparesheni za kulinda usalama baada ya kumalizika uchaguzi mkuu nchini humo.
Wizara ya Ulinzi wa Uganda imekadhibisha madai yaliyotolewa kupitia taarifa iliyochapishwa na gazeti moja la Uganda na kuyataja kuwa ni uwongo na yenye kupotosha. Wizara ya Ulinzi ya Uganda imekadhibisha taarifa hiyo iliyochapishwa katika gazeti la Sunday Pepper juzi Jumapili iliyodai kuwa jeshi la Uganda UPDF limejiweka tayari kusaidia oparesheni za usalama huko Kenya. Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Uganda aidha imekanusha ripoti kwamba Uganda ilituma wanajeshi wake baada ya kufanyika uchaguzi na kumhamishia Rais wa Kenya nchini Uganda.
Wizara hiyo imesema kuwa Kenya ni nchi inayojitawala na kwa msingi huo usalama wa nchi hiyo na watu wake unaihusu nchi hiyo yenyewe. Wizara ya Ulinzi ya Uganda imeongeza kuwa si serikali au jeshi la nchi hiyo lililopokea ombi la kutaka kutumwa wanajeshi huko Kenya na kwamba hakuna mazingira yanayoruhusu kuchukuliwa hatua kama hiyo.