Odinga kwenda Mahakama ya Juu Kenya kupinga matokeo ya urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33230-odinga_kwenda_mahakama_ya_juu_kenya_kupinga_matokeo_ya_urais
Kinara wa muungano wa upinzani wa NASA nchini Kenya, Raila Odinga hatimaye amepasua mbarika na kusema kuwa ataenda katika Mahakama ya Juu ya nchi kupinga matokeo ya kura za urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Aug 16, 2017 11:18 UTC
  • Odinga kwenda Mahakama ya Juu Kenya kupinga matokeo ya urais

Kinara wa muungano wa upinzani wa NASA nchini Kenya, Raila Odinga hatimaye amepasua mbarika na kusema kuwa ataenda katika Mahakama ya Juu ya nchi kupinga matokeo ya kura za urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.

Akihutubia waandishi wa habari jijini Nairobi hii leo, Odinga ambaye aligombea kiti hicho cha rais kwa mara ya nne amesema licha ya muungano huo kusisitiza hapo awali kuwa haitowasilisha kesi kotini kupinga matokeo hayo, lakini wameona kwenda mahakamani ni kwa maslahi yao na itakuwa fursa nzuri kufichua uchakachuaji uliotokea katika matokeo ya kura za rais.

Akiandamana na wakili wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na ambaye pia ni Seneta wa Siaya, James Orengo, kinara mwenza wake na pia Naibu wake, Kalonzo Musyoka na kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Raila amekariri kuwa matokeo ya Tume Huru ya Uchaguizi na Mipaka IEBC yaliyompa ushindi Kenyatta yalikuwa yamechakachuliwa.

Odinga (Kushoto) na Rais Kenyatta

Matokeo rasmi ya IEBC yanaonyesha kuwa, Uhuru Kenyatta aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Jubilee alipata ushindi baada ya kujizolea kura zaidi ya milioni nane na laki mbili sawa na asilimia 54.27 ya kura zote, huku Odinga  aliyegombea kwa tiketi ya ODM akipata kura zaidi ya milioni 6 na laki saba, sawa na asilimia 44.74 ya kura zote.

Hata hivyo viongozi wa NASA wanadai kuwa, Odinga alipata kura zaidi ya milioni nane huku Rais Kenyatta aliyewania kiti hicho kwa muhula wa pili akipata kura milioni saba na laki saba.