Mji wa Bariire Somalia wakombolewa kutoka mikononi mwa wanamgambo wa al-Shabab
Jeshi na Somalia likishirikiana na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM vimefanikiwa kuukomboa mji wa kiistratejia wa Bariire wa kusini mwa nchi hiyo uliokuwa ukidhibitiwa na wanamgambo wa kigaidi wa al-Shabab.
Naibu Gavana wa mkoa wa Lower Shebelle ameziambia duru za habari kwamba, mji huo umekombolewa baada ya operesheni kali ya pamoja ya jeshi la Somalia na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanamgambo wa al-Shabab waliokuwa wakiyadhibiti maeneo ya mji huo, wanmelazimika kuondoka baada ya kuzidiwa na operesheni ya kijeshi dhidi yao.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni jeshi la serikali ya Somalia limeshadidisha operesheni zake dhidi ya kundi la wanamgambo wa al-Shabab.
Wiki iliyopita, mapigano makali kati ya wanachama wa kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabab na wapiganaji watiifu kwa Mukhtaar Robow, kinara wa zamani wa kundi hilo huko kusini magharibi mwa Somalia yalipelekea kwa akali watu 20 kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Kundi la kigaidi la al-Shabab lilianzisha mashambulizi yake nchini Somalia mwaka 2006 ambapo baada ya mashambulizi ya jeshi la serikali ya nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMlSOM, lililazimika kukimbia kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu na kuelekea katika maeneo mengine ya mbali. Wanamgambo hao wangali wanadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na hivyo kuzidi kuhatarisha usalama wa Somalia inayokabiliwa pia na tatizo na ukame na njaa.