Wakimbizi 70,000 warejea kwa hiari Somalia kutoka Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33596-wakimbizi_70_000_warejea_kwa_hiari_somalia_kutoka_kenya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema limewarejesha nyumbani wakimbizi 70,516 wa Somalia kutoka Kenya, tangu kazi hiyo ianze mwaka 2014.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2017 01:59 UTC
  • Wakimbizi 70,000 warejea kwa hiari Somalia kutoka Kenya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema limewarejesha nyumbani wakimbizi 70,516 wa Somalia kutoka Kenya, tangu kazi hiyo ianze mwaka 2014.

Shirika hilo limesema wakimbizi 68,697 katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab pekee, kaskazini mashariki mwa Kenya,  wamerejea Somalia kwa hiari. Kambi ya Dadaab ambayo ina wakimbizi zaidi ya laki tatu iko kwenye mpaka wa Kenya na Somalia inahesabiwa kuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.

Aidha mwaka huu wakimbizi 29,383 wamerudi Somalia, na sasa bado kuna wakimbizi 18,274 waliojiandikisha wanaotaka kurudi Somalia.

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab

Tokea vita vianze Somalia mwaka 1992, Wasomali zaidi ya milioni mbili wamekimbia nchi yao ambapo milioni 1.1 ni wakimbizi ndani ya nchi na wengine laki 9 wamekimbilia nchi jirani.

Serikali ya Kenya imekuwa ikishinikiza UNHCR kufunga kambi ya Dadaab kwa sababu ya kile inachokitaja kuwa ni kutumiwa kambi hiyo kama ngome ya magaidi wa al-Shabab.