Wanajeshi wa Marekani waua watoto 3 katika hujuma Somalia
Raia wasiopungua 10, wakiwemo watoto watatu, wameuawa katika hujuma ya pamoja na Jeshi la Marekani na Jeshi la Somalia kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Taarifa zinasema hujuma hiyo ilitekelezwa mapema Ijumaa na kulenga shamba nje kidogo ya mji wa Bariire katika eneo la Lower Shabelle kusini mwa Somalia.
Naibu Gavana wa eneo hilo Ali Nur Mohamed amewaambia waandishi habari mjini Mogadishu kwamba, wakulima katika eneo hilo wanasema walivamiwa na wanajeshi wa kigeni wakati wakiwa shambani. Amesema kwa kuzingatia kuwa wakulima hao hawakuwa na silaha, wanajeshi hao wangewakamata badala ya kuwafyatulia risasi bila huruma. Aidha amesema watoto watatu na mwanamke ni kati ya waliopigwa risasi na kuuawa katika hujuma hiyo ya askari wa Marekani. Awali jeshi la Somalia lilidai kuwa hakuna raia aliyeuawa katika shambulio hilo na kwamba wote waliofariki walikuwa wafuasi wa kundi la kigaidila al-Shabab lakini baadaye limekiri kuwa raia kadhaa waliuawa.
Kamandi ya Jeshi la Marekani Afrika imethibitisha kuwa wanajeshi wa Marekani walihusika katika hujuma hiyo nchini Somalia pasina kutoa maelezo zaidi. Mapema mwaka huu Rais Donald Trump wa Marekani aliamuru kuimarisha oparesheni za kijeshi dhidi ya kundi la al-Shabab.
Tukio hilo linatazamiwa kuibua maswali mengi kuhusu ongezeko la harakati za kijeshi za Marekani nchini Somalia. Kwa kuzingatia kuwa askari wa kulinda amani wa Afrika maarufu kama AMISON wanatekeleza oparesheni dhidi ya al-Shabab nchini Somalia, weledi wa mambo wanasema kuimarisha kikosi hicho kutaweza kurejesha usalama kamili katika nchi hiyo na kwamba kuwepo wanajeshi wa Marekani kutayapa visingizio makundi yenye misimamo mikali.