UN: Watu milioni 3.8 wamefurushwa makwao kutokana na machafuko DRC
Umoja wa Mataifa umesema idadi ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliolazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko na mapigano nchini humo imeongezeka maradufu.
George Okoth-Obbo, afisa katika Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR jana Jumamosi alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita, wakimbizi wa Kongo DR wameongezeka na kupindukia milioni tatu na laki nane.
Amesema raia 33 elfu wa Kongo DR wamekimbilia Angola, wakitokea eneo la Kasai.
Afisa huyo wa UNHCR ameongeza kuwa, Kongo DR kadhalika inasumbuliwa na idadi kubwa ya wakimbizi wanaotoka nje ya nchi, na kwamba tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, nchi hiyo imepokea wakimbizi zaidi ya 60 elfu kutoka Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda na Sudan Kusini.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilitangaza habari ya kuweko wakimbizi milioni mbili katika mikoa ya Tanganyika, mashariki mwa nchi na Kasai, katikati mwa nchi hiyo.
Tangu mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa, watu zaidi ya 3,300 wameuawa huku wengine milioni 1.4 wakilazimika kuyakimbia makazi yao katika mapigano baina ya wanamgambo wanaomuunga mkono Kamwina Nsapu, kiongozi wa kundi la waasi katika eneo hilo na askari wa serikali ya nchi hiyo.