Wasomali wakataa kuzika watu wao mpaka serikali ikiri ilihusika na mauaji yao
Familia za Wasomali zimekataa kuzika maiti za wapendwa wao 10 wakiwemo watoto watatu mpaka serikali ikubali kubeba dhima ya mauaji yao yaliyofanywa katika shambulio lililotekelezwa kwa msaada wa jeshi la Marekani.
Watu hao 10 waliuliwa kwa kupigwa risasi wakati jeshi la Somalia likisaidiwa na askari wa Marekani lilipofanya operesheni ya shambulio katika kijiji cha Bariire kilichoko kilomita zipatazo 50 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Ali Nur Mohamed, naibu gavana wa eneo la Shabelle Chini amevieleza vyombo vya habari kuwa viwiliwili hivyo vitahifadhiwa mpaka serikali ilipe fidia.
"Tulikataa kuwazika kwa sababu serikali haijakubali; na hadi sasa bado haijakiri moja kwa moja kwamba iliua raia", ameeleza Nur.
Amesisitiza kuwa serikali ya Mogadishu inapaswa ikiri kwamba iliwaua raia kisha ilipe fidia.
Kwa mujibu wa naibu huyo gavana wa Shabelle Chini mamlaka husika zimetenga lori lenye kuhifadhi ubaridi la kuwekea kaa litumike kama mochuari ya kuhifadhia maiti hizo.
Kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika ilitangaza siku ya Ijumaa kuwa vikosi vyake vilishiriki kwa kutoa msaada kwenye operesheni ya kijeshi iliyofanywa na jeshi la Somalia kwenye kijiji cha Bariire na kueleza baadaye kuwa inachunguza ripoti kwamba kuna raia waliouawa katika operesheni hiyo.
Awali jeshi la Somalia lilitangaza kuwa watu wote waliouliwa katika shambulio hilo la Ijumaa walikuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Ash-Shabaab linalopambana nalo kwa msaada wa Marekani na vikosi vya Umoja wa Afrika AMISOM, lakini baadaye lilikiri kuwa baadhi ya raia pia waliuawa katika shambulio hilo.
Tukio hilo linatazamiwa kuibua maswali mengi kuhusu ongezeko la harakati za kijeshi za Marekani nchini Somalia. Kwa kuzingatia kuwa askari wa AMISOM wanatekeleza oparesheni dhidi ya al-Shabab nchini Somalia, weledi wa mambo wanasema kuimarisha kikosi hicho kutaweza kurejesha usalama kamili katika nchi hiyo na kwamba kuwepo wanajeshi wa Marekani kutayapa visingizio makundi yenye misimamo mikali ya kuhalalisha hujuma zao kwa hoja ya kupambana na majeshi vamizi ya Marekani.../