Wahajiri haramu 300 waokolewa katika pwani ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33782-wahajiri_haramu_300_waokolewa_katika_pwani_ya_libya
Kikosi cha gadi ya pwani ya Libya kimewaokoa wahajiri zaidi ya 300 katika maji ya magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 29, 2017 10:29 UTC
  • Wahajiri haramu 300 waokolewa katika pwani ya Libya

Kikosi cha gadi ya pwani ya Libya kimewaokoa wahajiri zaidi ya 300 katika maji ya magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.

Msemaji wa vikosi vya wanamaji wa Libya ametangaza kuwa walinzi wa pwani ya nchi hiyo mapema leo asubuhi waliwaokoa wahajiri haramu 140 magharibi mwa Tripoli na wengine 164 wakiwemo wanawake saba na watoto sita waliokolewa katika eneo la Sabratha.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, wahajiri hao wanajumuisha raia kutoka nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara, Misri, Morocco na Tunisia.

Katika miaka ya karibuni, mamia ya maelfu ya wahajiri kutoka Afrika na Mashariki ya Kati wamekuwa wakivuka jangwa la Libya na kuabiri kwenye mitumbwi tete na boti nyepesi katika bahari ya Mediterania kwa matumaini ya kufika barani Ulaya.

Kikao cha Paris cha kujadili suala la wahajiri

Makubaliano maalumu yalifikiwa hapo jana mjini Paris, Ufaransa kati ya nchi nne za Ulaya na tatu za Kiafrika ikiwemo Libya kuyasaidia mataifa yanayokabiliwa na kibarua cha kudhibiti mmiminiko wa raia wa kigeni.

Viongozi kutoka Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania na wenzao wa Libya, Niger na Chad walikubaliana kuweka utaratibu utakaowezesha kuwatambua wahajiri halali wanaokimbia vita na mateso na kuutumia Umoja wa Mataifa uwaorodheshe raia hao katika nchi za Niger na Chad ili kuwaepusha na kutumiwa vibaya na wafanya magendo ya binadamu.../