Sep 09, 2017 07:57 UTC
  • Vyama vya upinzani Angola vyaenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi

Vyama vitatu vya upinzani nchini Angola vimewasilisha malalamiko mahakamani dhidi ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo hivi karibuni, ambapo chama tawala cha MPLA kilitangazwa kuibuka mshindi.

Mbali na chama kikuu cha upinzani cha UNITA, vyama vingine vilivyowasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Katiba mjini Luanda jana Ijumaa ni FNLA na PNS, huku chama kingine cha upinzani cha Casa-CE kikitazamiwa kuelekea kortini leo Jumamosi.

Mkurugenzi wa Kampeni wa chama cha UNITA, Ruben Sikato aliwaambia waandishi wa habari hapo jana kuwa, sheria za uchaguzi zilikiukwa katika mikoa 15 kati ya ya 18ya nchi hiyo na kwamba wanaitaka mahakama itoe agizo la kuhesabiwa upya kura zilizopigwa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Isaias Samakuva, kinara wa chama kikuu cha upinzani nchini Angola alisema chama chake cha UNITA kinapinga vikali matokeo ya uchaguzi mkuu huo kutokana na uchakachuaji uliofanywa na maafisa wa Tume ya Uchaguzi nchini, akisisitiza kuwa,  matokeo ya awali ya Tume ya Uchaguzi Angola CNE, hayaendani na matokeo ya chama hicho kwa kuwa chama hicho kiliendesha zoezi la kujumlisha matokeo ya kura.

Rais anayeondoka wa Angola, Jose Eduardo Dos Santos

Jumatano iliyopita, Tume ya Uchaguzi ya Angola ilitangaza kuwa, chama tawala cha MPLA kilipata asilimia 61 ya kura na hivyo kuwa mshindi wa uchaguzi huo wa Agosti 23, huku chama cha UNITA kikitangazwa kuzoa aslimia 26.6 ya kura hizo. Kwa mujibu wa tume hiyo, MPLA ilizoa viti 150 kati ya 220 vya Bunge la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta.

Hii inaamisha kuwa, mgombea urais wa tiketi ya chama cha MPLA, Joao Lourenco, ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa Angola mwenye uhusiano wa karibu na Rais Jose Eduardo Dos Santos aliyestaafu, alishinda katika uchaguzi huo, na kumaliza kipindi cha zaidi ya miaka 38 ya uongozi wa Dos Santos.

Tags