Majaji wasitisha mgomo wa miezi minne nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34159-majaji_wasitisha_mgomo_wa_miezi_minne_nchini_sudan_kusini
Majaji na mahakimu nchini Sudan Kusini wametangaza kusitisha mgomo wao wa miezi minne baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kuahidi kutimiza matakwa yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 10, 2017 03:12 UTC
  • Majaji wasitisha mgomo wa miezi minne nchini Sudan Kusini

Majaji na mahakimu nchini Sudan Kusini wametangaza kusitisha mgomo wao wa miezi minne baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kuahidi kutimiza matakwa yao.

Bol Lul, Mwenyekiti wa Muungano wa Majaji na Mahakimu nchini humo amesema wameamua kusitisha mgomo wao uliodumu kwa takriban miezi minne, na watarejea kazini kuanzisha kesho Jumatatu pasina masharti.

Amesema muungano huo umeamua kutanguliza maslahi ya wananchi, na kwamba wameamua kurejea kazini kushughulikia mrundiko wa kesi za tangu mwezi Mei, walipoanza mgomo huo.

Miongoni mwa mambo yaliyowapelekea majaji hao kuitisha mgomo huo ni kushinikiza nyongeza ya mshahara, kuboreshwa mazingira ya kufanyia kazi pamoja na kulalamikia kupigwa kalamu nyekundu Jaji Mkuu Chan Reec Madut. 

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Katika makubaliano kati ya Rais Kiir na Muungano wa Majaji na Mahakimu, majaji 14 waliofutwa kazi kwa kushiriki maandamano ya kushinikiza matakwa yao mwezi Julai mwaka huu watarejeshwa kazini.

Mamlaka ya Huduma za Magereza nchini Sudan Kusini imekuwa ikilalamikia idadi kubwa ya watuhumiwa ambao wamezuiliwa wakisubiri kusikilizwa kesi zao.