Watu sita wauawa katika hujuma ya kigaidi Beledweyne Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34165-watu_sita_wauawa_katika_hujuma_ya_kigaidi_beledweyne_somalia
Watu wasiopungua sita wameuawa leo Jumapili baada ya gaidi mmoja kujiripua katika mkahawa ulioko nje ya ofisi ya kiserikali katika mji wa Beledweyne kati mwa Somalia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 10, 2017 09:54 UTC
  • Watu sita wauawa  katika hujuma ya kigaidi Beledweyne Somalia

Watu wasiopungua sita wameuawa leo Jumapili baada ya gaidi mmoja kujiripua katika mkahawa ulioko nje ya ofisi ya kiserikali katika mji wa Beledweyne kati mwa Somalia.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limedai kuhusika na hujuma hiyo.

Afisa wa ngazi za juu wa polisi katika eneo hilo, Meja Hussein Osman amethibitisha kutokea shambulizi hilo na kusema kuwa, watu sita walipoteza maisha wakati gaidi aliyekuwa amejifunga mshipi wa mabomu alipojiripua ndani ya mkahawa.

Hujuma huyo ya Jumapili alasiri nje ya ofisi ya gavana wa eneo la Hiran. Msemaji wa operesheni za kijeshi wa al Shabaab, Abdiasis Abu Musab amesema hujuma yao ilikuwa inalenga wafanyakazi wa serikali ya eneo la Hiran katika mji huo wa Beledweyne ulioko katika umbali wa kilomita 340 kaskazini mwa Mogadishu.

Walioshuhudia wanasema, kati ya waliopoteza maisha ni wazee wa ukoo katika eneo hilo. Kundi la kigaidi la ash-Shabab lilianzisha mashambulizi yake nchini Somalia mwaka 2006 ambapo katika mashambulizi ya jeshi la serikali ya nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMlSOM, lililazimika kukimbia kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu na kuelekea maeneo mengine ya mbali. Kundi hilo la wakufurishaji linalenga kuindoa madarakani serikali ya sasa ya Somalia.