Indhari yatolewa kuhusu unyanyasaji wanaofanyiwa watoto wakimbizi wa Kiafrika barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34253-indhari_yatolewa_kuhusu_unyanyasaji_wanaofanyiwa_watoto_wakimbizi_wa_kiafrika_barani_ulaya
Taasisi kadhaa mashuhuri za kimataifa zimetangaza kuwa watoto wahajiri wa Kiafrika wanakabiliwa na matatizo makubwa yakiwemo ya kufanyishwa kazi kwa nguvu, kupigwa na kutusiwa na kutumiwa vibaya kijinsia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2017 03:18 UTC
  • Indhari yatolewa kuhusu unyanyasaji wanaofanyiwa watoto wakimbizi wa Kiafrika barani Ulaya

Taasisi kadhaa mashuhuri za kimataifa zimetangaza kuwa watoto wahajiri wa Kiafrika wanakabiliwa na matatizo makubwa yakiwemo ya kufanyishwa kazi kwa nguvu, kupigwa na kutusiwa na kutumiwa vibaya kijinsia.

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF), taasisi za uhajiri zilizo chini ya umoja huo pamoja na Shirika la Kimataifa la Uhajiri yametoa ripoti ya pamoja mapema leo na kutangaza kuwa watoto wanaotoka nchi za eneo la Jangwa la Sahara barani Afrika wanakabiliwa zaidi na vitendo vya kufanyishwa kazi kwa nguvu, kupigwa na kutusiwa na kutumiwa vibaya kijinsia kuliko watoto wa maeneo mengine ya dunia waliolazimika kuhama makwao na kukimbilia nchi za Ulaya.

Watoto wakimbizi kutoka nchi za Afrika

Kwa mujibu wa ripoti hiyo karibu asilimia 83 ya watoto wanaotoka nchi za eneo la jangwa la Sahara barani Afrika wanaoelekea Ulaya kupitia Libya wanakabiliwa na hatari ya kutumiwa vibaya, wakati kiwango cha watoto wa mataifa mengine wanaokabiliwa na hatari hiyo ni asilimia 56.

Idadi ya watoto wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi na waliobaki bila makaazi imefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, ambapo katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2016 watoto laki tatu wasio na waliofuatana nao na waliotenganishwa na wazazi wao wamesajiliwa katika nchi 80 duniani.../