Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC ataka kutiwa mbaroni kamanda wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34341-mwendesha_mashtaka_mkuu_wa_icc_ataka_kutiwa_mbaroni_kamanda_wa_libya
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) amekariri wito wake wa kutiwa mbaroni haraka iwezekanavyo kamanda wa ngazi ya juu huko Libya anayesakwa kwa jinai za kivita. Kamanda huyo anatuhumiwa kuwaua watu wengi.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 14, 2017 03:24 UTC
  • Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC ataka kutiwa mbaroni kamanda wa Libya

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) amekariri wito wake wa kutiwa mbaroni haraka iwezekanavyo kamanda wa ngazi ya juu huko Libya anayesakwa kwa jinai za kivita. Kamanda huyo anatuhumiwa kuwaua watu wengi.

Bi Fatou Bensouda amesema kuwa, Mahmoud Mustafa Busayf Al-Werfalli anatuhumiwa kwa jinai nyingi kwa msingi huo ametoa wito kwa Libya kwa mara nyingine tena kuchukua hatua zote zinazowezekana kumtia mbaroni haraka na kumkabidhi kwa ICC.

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama ya ICC 

Al Werfalli ambaye alizaliwa mwaka 1978 ni kamanda wa ngazi ya juu katika brigedi ya Al- Saiqa iliyojitenga na Jeshi la Taifa la Libya baada ya kuibuka mapambano ya kumng'oa madarakani dikteta wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mwaka 2011.  Brigedi hiyo imekuwa ikipigana bega kwa bega na wapiganaji watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar huko Benghazi; mji wa pili kwa ukubwa wa Libya ambao umekombolewa hivi karibuni baada ya mapigano ya miaka mitatu. Majaji wa Mahakama ya ICC mwezi Agosti mwaka huu walitoa waranti wa kutiwa mbaroni Al Werfalli wakidai kuwa amehusika na mauaji ya watu 33 katika mji huo.