Museveni: Kikomo cha umri wa kuwania urais Uganda kitaamuliwa na Bunge
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34357-museveni_kikomo_cha_umri_wa_kuwania_urais_uganda_kitaamuliwa_na_bunge
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amejitosa kwenye mjadala kuhusu kikomo cha umri wa kugombea urais nchini humo na kusisitiza kuwa, kauli ya mwisho kuhusu kadhia hiyo itatolewa na Bunge la nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 14, 2017 10:14 UTC
  • Museveni: Kikomo cha umri wa kuwania urais Uganda kitaamuliwa na Bunge

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amejitosa kwenye mjadala kuhusu kikomo cha umri wa kugombea urais nchini humo na kusisitiza kuwa, kauli ya mwisho kuhusu kadhia hiyo itatolewa na Bunge la nchi hiyo.

Rais Museveni amesema sheria iko wazi kuhusu mchakato wa kufanyiwa marekebisho Katiba ya nchi na kubadili kipengee chochote na anatumai kuwa Wabunge wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki watafuata taratibu zilizopo.

Tayari Wabunge wa chama tawala NRM wameafikiana kuwasilisha Bungeni muswada unaotaka kukifanyia mabadiliko kipengee cha 102 (b) cha Katiba ya Uganda, ambacho kinaainisha kuwa, umri ambao mtu anaweza kuwania urais nchini humo ni kati ya miaka 35 na 75.

Rais Museveni atakuwa na umri wa miaka 76 wakati wa uchaguzi ujao nchini Uganda mwaka 2021 na iwapo marekebisho hayo ya Katiba yataidhinishwa, basi ataweza kuvuka kiunzi hicho cha umri.

Dakta Kizza Besigye, kiongozi wa upinzani Uganda

Mbali na wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na kinara wao, Kizza Besigye kukosoa vikali muswada huo, wabunge wanne wanaotajwa kuwa waasi wa chama tawala NRM pia wameonekana kutokubaliana na wazo hilo la Museveni kuruhusiwa kushiriki uchaguzi ujao.

Wakati huo huo, Rais Museveni amepuuzilia mbali kauli aliyoitoa mwaka 2012 kwamba mtu akifikisha miaka 75 anakosa tena haiba na nguvu za kuongoza taifa kama Rais, mara hii akisisitiza kuwa, suala hilo ni la kiafya na madaktari tu ndio wanaweza kuamua iwapo mtu akifikisha miaka 75 ana uwezo wa kiafya wa kuongoza au la.

Ifahamike kuwa, Rais Yoweri Kaguta Museveni amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 ambapo kwa sasa anahudumu muhula wake wa tano.