Wabunge wa upinzani Uganda wadai kutishiwa maisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34637-wabunge_wa_upinzani_uganda_wadai_kutishiwa_maisha
Wabunge wa vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema serikali inawatishia maisha masaa machache kabla ya bunge la nchi hiyo kujadili muswada wa kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2017 23:18 UTC
  • Wabunge wa upinzani Uganda wadai kutishiwa maisha

Wabunge wa vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema serikali inawatishia maisha masaa machache kabla ya bunge la nchi hiyo kujadili muswada wa kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais nchini humo.

Wabunge hao wamesema maafisa usalama wameenea katika mji mkuu Kampala hususan nje ya majengo ya bunge, huku Wabunge wakitazamiwa kuujadili muswada huo leo Alkhamisi.

Wabunge wa upinzani John Baptist Nambeshe na Wilfred Niwagaba wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kitendo hicho cha kutia hofu miongoni mwa wananchi na watunga sheria hakitawateteresha na watahakikisha kuwa muswada huo haufui dafu.

Richard Karemire, Msemaji wa Jeshi la Uganda amesema hatua ya wao kuimarisha usalama si ngeni na kwamba wamekuwa wakifanya hivyo mara kwa mara.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda mwenye miaka 73

Wabunge wa chama tawala NRM wameafikiana kuwasilisha Bungeni muswada unaotaka kukifanyia mabadiliko kipengee cha 102 (b) cha Katiba ya Uganda, ambacho kinaainisha kuwa, umri ambao mtu anaweza kuwania urais nchini humo ni kati ya miaka 35 na 75.

Rais Museveni atakuwa na umri wa miaka 76 wakati wa uchaguzi ujao nchini Uganda mwaka 2021 na iwapo marekebisho hayo ya Katiba yataidhinishwa, basi ataweza kuvuka kiunzi hicho cha umri.

Mbali na wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na kinara wao, Kizza Besigye kukosoa vikali muswada huo, wabunge wanne wanaotajwa kuwa waasi wa chama tawala NRM pia wameonekana kutokubaliana na wazo hilo la Museveni kuruhusiwa kushiriki uchaguzi ujao.