UN: Wafuasi wa Gaddafi wanaweza kushiriki katika siasa za Libya
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya amesema kuwa, makundi yote ya nchi hiyo wakiwemo wafuasi wa dikteta wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi wanaweza kushiriki katika mwenendo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Ghassan Salamé amesema kuwa makundi yote ya kisiasa yanapaswa kuruhusiwa kushiriki katika chaguzi za Bunge na Rais nchini Libya.
Ameongeza kuwa, kuwa ulazima wa kutayarishwa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi nchini Libya na hatua ya kwanza kabisa ni kutayarisha sheria za uchaguzi kwa sababu hadi sasa hakujawahi kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo.
Ghassan Salamé ametahadhafrisha kuhusu mpango wowote wa kutatua mgogoro wa nchi hiyo bila ya kuushirikisha Umoja wa Mataifa.
Libya ilitumbukia katika vita na machafuko ya ndani baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi. Kwa sasa nchi hiyo inaongozwa na serikali mbili zinazopingana.