Kabila: Congo DR inaelekea kwenye uchaguzi wa wazi na wa amani
(last modified Sat, 23 Sep 2017 15:59:22 GMT )
Sep 23, 2017 15:59 UTC
  • Kabila:  Congo DR inaelekea kwenye uchaguzi wa wazi na wa amani

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa nchi hiyo inaelekea kwenye uchaguzi wa kuaminika, wa wazi na wa amani.

Kabila ameyasema hayo leo katika hotuba yake kwenye mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Matamshi hayo ya Kabila yametolewa baada ya wimbi kubwa la malalamiko ya ndani na nje ya nchi hiyo linalomlaumu kwa kuendelea kung'angania madaraka na baada ya taasisi za serikali ya Kinshasa kuashiria kwamba huenda uchaguzi wa rais usifanyike nchini huko mwishoni mwa mwaka huu kwa mujibu wa makubaliano ya serikali na kambi ya upinzani.

Rais wa Congo amesisitiza katika hotuba hiyo kwamba atahakikisha kuwa wale waliohusika na mauaji ya watafiti wawili wa Umoja wa Mataifa nchini Congo mapema mwaka huu wanaadhibiwa.

Zaida Catalan na Michael Sharp

Amesema: Kinshasa itafanya uchunguzi kuhusu hali halisi ya uhalifu huo na kuhakikisha kuwa kitendo hicho cha kutisha hakipiti hivihivi bila ya wahusika kuadhibiwa.

Mmarekani, Michael Sharp, aliyekuwa mratibu wa kundi linalosimamia vikwazo, na raia wa Sweden, Zaida Catalan waliuawa tarehe 12 Machi mwaka huu nchini Congo wakifanya uchunguzi kwa ajili ya ripoti iliyopangwa kuwasilishwa katika Umoja wa Mataifa.