Kenya kukabiliana na maandamano ya wapinzani
Serikali ya Kenya imesema maandamano ya muungano wa upinzani Nasa ambayo yamepangwa kuanza Jumatatu yatadhibitiwa na vitengo vya kuimarisha usalama vya nchi hiyo.
Katibu maalumu katika Wizara ya Usalama wa Ndani ya Kenya, Karanja Kibicho amesema leo Ijumaa kuwa maandamano ya muungano wa Nasa ambayo yamepangwa kuanza Jumatatu yatadhibitiwa na vitengo vya kudumisha usalama.
Amesema kuwa ni haki ya wafuasi wa Nasa na viongozi wao kujitokeza mitaani kutetea lolote linalowahusu bora tu katika kufanya hivyo wasisababishe fujo na matatizo kwa wengine wasio na imani na mrengo wao.
Akiongea katika Kaunti ya Kirinyaga eneo la katikati mwa Kenya, Kibicho amesema kuwa serikali haina nia yoyote ya kuzima maandamano hayo.
"Kile hatutakubali ni visa vya wahalifu kutatiza shughuli katika jamii kwa kisingizo cha kutetea haki na ajenda zao binafsi ndani ya Nasa,” amesema Kibicho.
Kibicho amewahakikishia wafanyabiashara katika miji yote ya nchini Kenya ambao hawana imani na maandamano hayo wajitokeze kama kawaida kufanya biashara zao akisema: “Serikali katika wajibu wake wa kulinda roho na mali, itakuwajibikia vilivyo.”
Muungano wa upinzani nchini Kenya Nasa umesema kuwa, utaongoza maandamano ya wafuasi wake nje ya Ofisi ya Tume ya Uchaguzi jijini Nairobi, kushinikiza mabadiliko ndani ya tume hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio wa urais tarehe 26 mwezi ujao wa Oktoba.
Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga ametangaza kuwa, hawatakubali kufanyika uchaguzi huo iwapo Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Ezra Chiloba na maafisa wengine wataendelea kuandaa uchaguzi mpya ambao utakuwa ni mchuano kati ya Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.