Al-Shabaab: Tumeua wanajeshi 73 wa Somalia, Lower Shabelle
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i3529-al_shabaab_tumeua_wanajeshi_73_wa_somalia_lower_shabelle
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limedai kuwaua askari 73 wa jeshi la taifa la Somalia, katika makabiliano makali yaliyotokea jana huko Shabelle ya Chini, yapata kilomita 60 kusini mwa mji mkuu, Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2016 11:45 UTC
  • Magaidi wa al Shabab
    Magaidi wa al Shabab

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limedai kuwaua askari 73 wa jeshi la taifa la Somalia, katika makabiliano makali yaliyotokea jana huko Shabelle ya Chini, yapata kilomita 60 kusini mwa mji mkuu, Mogadishu.

Abdulaziz Abu Mus’ab, msemaji wa operesheni za al-Shabaab amenukuliwa na kanali ya televisheni ya al-Andalus inayomilikiwa na kundi hilo la kigaidi akidai kuwa, wanamgambo hao wa kitafiri wameua askari wote 73 wa kikosi cha 5 cha jeshi la Somalia, waliokuwa katika kambi ya jeshi ya Lanta Bur, katika eneo la Shabelle ya Chini. Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi hao wameiba magari 4 ya jeshi la Somalia na kuteketeza moto lori moja la kijeshi lililoharibika katika eneo la Awdegle, yapata kilomita 70 kusini magharibi mwa Mogadishu. Hata hivyo jeshi la Somalia halijatoa taarifa yeyote ya kukiri au kukanusha madai hayo ya magaidi wa al-Shabaab. Hii ni katika hali ambayo, hapo jana, Msemaji wa Jeshi la Kenya KDF Kanali David Obonyo alisema Jeshi la Kenya limewaangamiza magaidi 21 wa kundi la kitakfiri la al-Shabaab kufuatia mapigano makali yaliyojiri mjini Afmadow kusini mwa Somalia Jumamosi alasiri. Aidha Jumapili ya jana, jeshi la Kenya lilitangaza kuwaua magaidi 13 wa al-Shabaab katika eneo la Sarira katika Ukanda wa Lacta yapata kilomita 30 kaskazini mwa Ras Kamboni. Vikosi vya Kenya vilinasa silaha kadhaa katika oparesheni hiyo.